Yeremia 10
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Sikieni lile ambalo Bwana, anena nanyi ee nyumba ya Israeli.
2Hili ndilo asemalo Bwana: “Usijifunze njia za mataifa wala usitishwe na ishara katika anga, ingawa mataifa yanatishwa nazo.
3Kwa maana desturi za mataifa hazina maana, wanakata mti msituni, na fundi anauchonga kwa patasi.
4Wanaparemba kwa fedha na dhahabu, wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike.
5Sanamu zao ni kama sanamu iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege nazo haziwezi kuongea; sharti zibebwe sababu haziwezi kutembea. Usiziogope; haziwezi kudhuru, wala kutenda lolote jema.”
6Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana; wewe ni mkuu, jina lako ni lenye nguvu katika uweza.
7Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe, Ee Mfalme wa mataifa? Hii ni stahili yako. Miongoni mwa watu wote wenye hekima katika mataifa na katika falme zao zote, hakuna aliye kama wewe.
8Wote hawana akili, tena ni wapumbavu, wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote.
9Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi na dhahabu kutoka Ufazi. Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani: vyote vikiwa vimetengenezwa na mafundi stadi.
10Lakini Bwana ni Mungu wa kweli, yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. Anapokasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
11“Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ”
12Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake, akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake, na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
13Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma; huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua, naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
14Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa, kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu, havina pumzi ndani yavyo.
15Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha tu, hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia.
16Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, pamoja na Israeli, kabila la urithi wake: Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.
17Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii, enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
18Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu wote waishio katika nchi hii; nitawataabisha ili waweze kutekwa.”
19Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu! Jeraha langu ni kubwa! Lakini nilisema, “Kweli hii ni adhabu yangu, nami sharti niistahimili.”
20Hema langu limeangamizwa; kamba zake zote zimekatwa. Wana wangu wametekwa na hawapo tena; hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu wala wa kusimamisha kibanda changu.
21Wachungaji hawana akili wala hawamuulizi Bwana, hivyo hawastawi na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.
22Sikilizeni! Taarifa inakuja: ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini! Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa, makao ya mbweha.
23Ninajua, Ee Bwana, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe; hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
24Unirudi, Ee Bwana, lakini kwa kipimo cha haki: si katika hasira yako, usije ukaniangamiza.
25Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa wasiokujua wewe, juu ya mataifa wasioliitia jina lako. Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo; wamemwangamiza kabisa na kuiharibu nchi yake.
Yeremia
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License