Yeremia 21

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Neno lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana wakati Mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkiya, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwake, kusema:

2“Tuulizie sasa kwa Bwana, kwa sababu Nebukadneza mfalme wa Babeli anatushambulia. Labda Bwana atatenda maajabu kwa ajili yetu kama nyakati zilizopita, ili Nebukadneza atuondokee.”

3Lakini Yeremia akawajibu, “Mwambieni Sedekia,

4‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kuwageuzia silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo mnatumia kupigana na mfalme wa Babeli na Wakaldayo ambao wako nje ya ukuta wakiwazunguka kwa jeshi. Nami nitawakusanya ndani ya mji huu.

5Mimi mwenyewe nitapigana dhidi yenu kwa mkono wangu ulionyooshwa na mkono wa nguvu, kwa hasira na ghadhabu kali na ukali mwingi.

6Nitawaangamiza waishio katika mji huu, watu na wanyama, nao watauawa kwa tauni ya kutisha.

7Baada ya hayo, nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na watu wa mji huu ambao walinusurika tauni, upanga na njaa, mkononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, na kwa adui zao wale wanaotafuta uhai wao. Atawaua kwa upanga; hatakuwa na rehema juu yao au huruma wala kuwasikitikia,’ asema Bwana.

8“Zaidi ya hayo, waambie watu hawa, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama, naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.

9Yeyote atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni. Lakini yeyote atakayetoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo ambao wameuzunguka mji huu kwa jeshi, atanusurika, naye ataishi.

10Nimekusudia kuufanyia mji huu jambo baya, wala si jema. Utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto, asema Bwana.’

11“Zaidi ya hayo, ambia nyumba ya mfalme ya Yuda, ‘Sikia neno la Bwana,

12Ewe nyumba ya Daudi, hili ndilo Bwana asemalo: “ ‘Hukumuni kwa haki kila asubuhi, mwokoeni mikononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara, la sivyo ghadhabu yangu italipuka na kuwaka kama moto kwa sababu ya uovu mlioufanya: itawaka na hakuna wa kuizima.

13Niko kinyume nawe, ee Yerusalemu, wewe uishiye juu ya bonde hili kwenye uwanda wa juu wa miamba, asema Bwana, wewe usemaye, “Ni nani awezaye kuja kinyume chetu? Nani ataingia mahali pa kimbilio letu?”

14Nitawaadhibu kama istahilivyo matendo yenu, asema Bwana. Nitawasha moto katika misitu yenu ambao utateketeza kila kitu kinachowazunguka.’ ”

Yeremia

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License