Hosea 8
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1“Wekeni tarumbeta midomoni mwenu! Tai yuko juu ya nyumba ya Bwana kwa sababu watu wamevunja Agano langu, wameasi dhidi ya sheria yangu.
2Israeli ananililia, ‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’
3Lakini Israeli amekataa lile lililo jema, adui atamfuatia.
4Wanaweka wafalme bila idhini yangu, wamechagua wakuu bila kibali changu. Kwa fedha zao na dhahabu wamejitengenezea sanamu kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe.
5Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama! Hasira yangu inawaka dhidi yao. Watakuwa najisi mpaka lini?
6Zimetoka katika Israeli! Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu. Atavunjwa vipande vipande, yule ndama wa Samaria.
7“Wanapanda upepo na kuvuna upepo wa kisulisuli. Bua halina suke, halitatoa unga. Kama lingetoa nafaka, wageni wangeila yote.
8Israeli amemezwa; sasa yupo miongoni mwa mataifa kama kitu kisicho na thamani.
9Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake. Efraimu amejiuza mwenyewe kwa wapenzi.
10Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa, sasa nitawakusanya pamoja. Wataanza kudhoofika chini ya uonevu wa mfalme mwenye nguvu.
11“Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi kwa ajili ya sadaka za dhambi, hizi zimekuwa madhabahu za kufanyia dhambi.
12Nimeandika kwa ajili yao mambo mengi kuhusu sheria yangu, lakini wameziangalia kama kitu cha kigeni.
13Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi nao wanakula hiyo nyama, lakini Bwana hapendezwi nao. Sasa ataukumbuka uovu wao na kuadhibu dhambi zao: Watarudi Misri.
14Israeli amemsahau Muumba wake na kujenga majumba ya kifalme, Yuda amejengea miji mingi ngome. Lakini nitatuma moto kwenye miji yao utakaoteketeza ngome zao.”
Hosea
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License