Hosea 10
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana, alijizalia matunda mwenyewe. Kadiri matunda yake yalivyoongezeka, alijenga madhabahu zaidi; kadiri nchi yake ilivyostawi, alipamba mawe yake ya ibada.
2Moyo wao ni mdanganyifu, nao sasa lazima wachukue hatia yao. Bwana atabomoa madhabahu zao na kuharibu mawe yao ya ibada.
3Kisha watasema, “Hatuna mfalme kwa sababu hatukumheshimu Bwana. Lakini hata kama tungelikuwa na mfalme, angeweza kutufanyia nini?”
4Wanaweka ahadi nyingi, huapa viapo vya uongo wanapofanya mapatano; kwa hiyo mashtaka huchipuka kama magugu ya sumu katika shamba lililolimwa.
5Watu wanaoishi Samaria huogopa kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni. Watu wake wataiombolezea, vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu, wale waliokuwa wamefurahia fahari yake, kwa sababu itaondolewa kutoka kwao kwenda uhamishoni.
6Itachukuliwa kwenda Ashuru kama ushuru kwa mfalme mkuu. Efraimu atafedheheshwa; Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.
7Samaria na mfalme wake wataelea kama kijiti juu ya uso wa maji.
8Mahali pa kuabudia sanamu pa uovu pataharibiwa: ndiyo dhambi ya Israeli. Miiba na mibaruti itaota na kufunika madhabahu zao. Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!” na vilima, “Tuangukieni!”
9“Tangu siku za Gibea, mmetenda dhambi, ee Israeli, huko ndiko mlikobaki. Je, vita havikuwapata watenda mabaya huko Gibea?
10Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu; mataifa yatakusanywa dhidi yao ili kuwaweka katika vifungo kwa ajili ya dhambi zao mbili.
11Efraimu ni mtamba wa ngʼombe aliyefundishwa ambaye hupenda kupura, hivyo nitamfunga nira juu ya shingo yake nzuri. Nitamwendesha Efraimu, Yuda lazima alime, naye Yakobo lazima avunjavunje mabonge ya udongo.
12Jipandieni wenyewe haki, vuneni matunda ya upendo usio na kikomo, vunjeni ardhi yenu isiyolimwa; kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Bwana, mpaka atakapokuja na kuwanyeshea juu yenu haki.
13Lakini mmepanda uovu, mkavuna ubaya, mmekula tunda la udanganyifu. Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe na wingi wa mashujaa wenu,
14mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako, ili kwamba ngome zako zote zitaharibiwa: kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita, wakati mama pamoja na watoto wao walipotupwa kwa nguvu ardhini.
15Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli, kwa sababu uovu wako ni mkuu. Siku ile itakapopambazuka, mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.
Hosea
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License