Hosea 3

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Bwana akaniambia, “Nenda, ukaonyeshe upendo wako kwa mke wako tena, ingawa amependwa na mwingine naye ni mzinzi. Mpende kama Bwana apendavyo Waisraeli, ingawa wanageukia miungu mingine na kupenda mikate mitamu ya zabibu kavu iliyowekwa wakfu.”

2Basi nilimnunua huyo mwanamke kwa shekeli kumi na tano za fedha, pia kwa kiasi kama cha homeri moja na nusu ya shayiri.

3Kisha nilimwambia, “Utaishi nami kwa siku nyingi, hupaswi kuwa kahaba au kuwa na uhusiano wa karibu na mtu yeyote, nami nitaishi na wewe.”

4Kwa maana Waisraeli wataishi siku nyingi bila kuwa na mfalme wala mkuu, bila kuwa na dhabihu wala mawe matakatifu, bila kisibau wala sanamu.

5Baadaye Waisraeli watarudi na kumtafuta Bwana Mungu wao na Daudi mfalme wao. Watakuja wakitetemeka kwa Bwana na kwa baraka zake katika siku za mwisho.

Hosea

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License