Yoeli 1
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Neno la Bwana ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.
2Sikilizeni hili, enyi wazee; sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi. Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea katika siku zenu au katika siku za babu zenu?
3Waelezeni watoto wenu, na watoto wenu wawaambie watoto wao, na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.
4Kilichosazwa na kundi la tunutu nzige wakubwa wamekula, kilichosazwa na nzige wakubwa parare wamekula, kilichosazwa na parare madumadu wamekula.
5Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyangʼanywa kutoka midomoni mwenu.
6Taifa limevamia nchi yangu, lenye nguvu tena lisilo na idadi; lina meno ya simba, magego ya simba jike.
7Limeharibu mizabibu yangu na kuangamiza mitini yangu. Limebambua magome yake na kuyatupilia mbali, likayaacha matawi yake yakiwa meupe.
8Omboleza kama bikira aliyevaa nguo ya gunia anayehuzunika kwa ajili ya mume wa ujana wake.
9Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Bwana. Makuhani wanaomboleza, wale wanaohudumu mbele za Bwana.
10Mashamba yameharibiwa, ardhi imekauka; nafaka imeharibiwa, mvinyo mpya umekauka, mafuta yamekoma.
11Kateni tamaa, enyi wakulima, lieni, enyi mlimao mizabibu; huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri, kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.
12Mzabibu umekauka na mtini umenyauka; mkomamanga, mtende na mtofaa, miti yote shambani, imekauka. Hakika furaha yote ya mwanadamu imeondoka.
13Vaeni nguo ya gunia, enyi makuhani, muomboleze; pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni. Njooni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha, enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu; kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.
14Tangazeni saumu takatifu; liiteni kusanyiko takatifu. Iteni wazee na wote waishio katika nchi waende katika nyumba ya Bwana Mungu wenu, wakamlilie Bwana.
15Ole kwa siku hiyo! Kwa kuwa siku ya Bwana iko karibu; itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.
16Je, chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu: furaha na shangwe kutoka nyumba ya Mungu wetu?
17Mbegu zinakauka chini ya mabonge ya udongo. Ghala zimeachwa katika uharibifu, ghala za nafaka zimebomolewa, kwa maana hakuna nafaka.
18Jinsi gani ngʼombe wanavyolia! Makundi ya mifugo yanahangaika kwa sababu hawana malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka.
19Kwako, Ee Bwana, naita, kwa kuwa moto umeteketeza malisho ya mbugani na miali ya moto imeunguza miti yote shambani.
20Hata wanyama wa porini wanakuonea shauku; vijito vya maji vimekauka, na moto umeteketeza malisho yote ya mbugani.
Yoeli
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License