Mistari ya Biblia Kuhusu Hasira
Mistari 14 ya Biblia kuhusu Hasira ya kusoma, kutafakari, na kuikariri.
Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu.
Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, wala msimpe ibilisi nafasi.
Jawabu la upole hugeuza ghadhabu, bali neno liumizalo huchochea hasira.
Mtu mwenye subira ana ufahamu mwingi, bali anayekasirika haraka huonyesha upumbavu.
Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu.
Ni afadhali mtu mstahimilivu kuliko shujaa, mtu anayeitawala hasira yake kuliko yule autekaye mji.
Mpumbavu huonyesha hasira yake yote, bali mwenye hekima hujizuia.
Usiwe mwepesi kukasirika rohoni mwako, kwa kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.
Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.
Hekima ya mtu humpa uvumilivu, ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.
Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu?
Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana.
Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka, usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika, la sivyo utajifunza njia zake na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.