Ezekieli 2
Neno: Kiswahili Contemporary Version
Akaniambia, “Mwanadamu, simama kwa miguu yako nami nitasema nawe.”
Alipokuwa akiongea nami, Roho akanijia na kunisimamisha wima, nikamsikia akisema nami.
Akaniambia: “Mwanadamu, ninakutuma kwa Waisraeli, kwa taifa asi ambalo limeniasi mimi, wao na baba zao wananikosea mimi hadi leo.
Watu ambao ninakutuma kwao ni wapotovu na wakaidi. Waambie, ‘Hivi ndivyo anavyosema Bwana Mwenyezi.’
Kama watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi, watajua nabii amekuwa miongoni mwao.
Nawe mwanadamu, usiwaogope wao wala maneno yao, usiogope, ingawa michongoma na miiba vinakuzunguka na unaishi katikati ya nge. Usiogope yale wasemayo wala usitishwe nao, ingawa wao ni nyumba ya uasi.
Wewe lazima uwaambie maneno yangu, ikiwa wanasikiliza au hawasikilizi, kwa kuwa wao ni watu waasi.
Lakini wewe mwanadamu, sikiliza ninalokuambia. Usiwe mwenye kuasi kama hiyo nyumba ya kuasi. Fungua kinywa chako na ule nikupacho.”
Ndipo nikatazama, nami nikaona mkono ulionyooshwa kunielekea. Nao ulikuwa na ukurasa wa kitabu,
ambao aliukunjua mbele yangu. Pande zote mbili ulikuwa umeandikwa maneno ya maombolezo, vilio na ole.
Ezekieli
Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License