Mhubiri 10
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Kama vile nzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato, ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima.
2Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume, lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto.
3Hata anapotembea barabarani, mpumbavu hukosa ufahamu na kudhihirisha kwa kila mmoja jinsi alivyo mpumbavu.
4Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako, usiache mahali pako, utulivu huweza kuzuia makosa mengi.
5Kuna ubaya niliouona chini ya jua, aina ya kosa litokalo kwa mtawala:
6Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za juu, wakati matajiri hushika nafasi za chini.
7Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, wakati wakuu wakitembea kwa miguu kama watumwa.
8Yeye achimbaye shimo aweza kutumbukia ndani yake, yeyote abomoaye ukuta anaweza kuumwa na nyoka.
9Yeyote apasuaye mawe inawezekana yakamuumiza, yeyote apasuaye magogo inawezekana yakamuumiza.
10Kama shoka ni butu na halikunolewa, nguvu nyingi zinahitajika, lakini ustadi utaleta mafanikio.
11Kama nyoka akiuma kabla ya kufanyiwa uaguzi, mwaguzi hatahitajika tena.
12Maneno yatokayo kinywani mwa mtu mwenye hekima yana neema, bali mpumbavu huangamizwa na midomo yake mwenyewe.
13Mwanzoni maneno yake ni upumbavu, mwishoni ni wazimu mbaya,
14naye mpumbavu huzidisha maneno. Hakuna yeyote ajuaye linalokuja, ni nani awezaye kueleza ni jambo gani litakalotokea baada yake?
15Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe, hajui njia iendayo mjini.
16Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi.
17Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa: ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi.
18Kama mtu ni mvivu paa la nyumba huinama, kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja.
19Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, nao mvinyo hufurahisha maisha, lakini fedha ni jawabu la mambo yote.
20Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako, au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala, kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako, naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.
Mhubiri
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License